TUMAINI MAKUMIRA YASHIRIKI KONGAMANO LA IDHAA ZA KISWAHILI DUNIANI

Chuo kikuu Tumaini Makumira ni moja kati ya vyuo vikuu Tanzania ambavyo vinashiriki katika Kongamano hilo la 5 la Idhaa za Kiswahili Duniani lililoandaliwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), likiwakutanisha wadau wa Idhaa za Kiswahili kutoka ndani na nje ya nchi linalofanyika kuanzia tarehe 24 hadi 27 Machi, 2026 katika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC), Jijini Arusha.

Akizungumza katika ufunguzi huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Idhaa za Kiswahili zimekuwa ni mhimili muhimu wa maendeleo ya lugha ya kiswahili kwa kutoa taarifa sahihi, kuimarisha elimu, demokrasia na maadili ya jamii.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  amefahamisha kuwa mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii  yanayotokea yanaendelea kuifanya lugha ya kiswahili kuwa nyenzo muhimu ya mawasiliano, maarifa na maendeleo nchini. 

Amefahamisha kuwa Vyombo vya habari pamoja na majukwaa ya kidijitali kama vile mitandao ya kijami vina nafasi ya kipekee katika kuifikisha lugha ya kiswahili kwa hadhira pana zaidi duniani kupitia ubunifu wa kidijitali kama vile maudhui ya mitandao ya kijamii, video za elimu na program za simu . 

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewaagiza viongozi na watendaji wa Idhaa za Kiswahili kuendeleza utaratibu wa kukaa pamoja na wataalamu wa Kiswahili na kubadilishana uzoefu wa namna bora zaidi ya kukikuza kiswahili pamoja na kukabiliana na changamoto za utangazaji kwa kiswahili. 

Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) Profesa Martin Mhandoamesema BAKITA  itaendelea kutoa kila aina ya ushirikiano ili  kuhakikisha lugha ya kiswahili inaendelea kutumika kwa ufasaaha hasa katika vyombo vya habari na kuiwezesha lugha hio kuendana na Mabadiliko ya Kidunia. 

Profesa Mhando amefahamisha kuwa Idhaa za Kiswahili Dunianiz zimekuwa na mchango mkubwa katika zikiifikia hadhira na kukitangaza kiswahili Kimataifa hivyo zinapaswa kuhakikisha wanakitumia kiswahili kwa ufasaha wakati wa kufikisha  ujumbe kwa hadhira iliyokusudiwa.